Imani hii ambayo haina dini iliyosajiliwa inanifanya nikubaliane na mtazamo wangu wa kupinga wasanii wa muziki wanaoimba kwa kufuatisha nyimbo zao jukwaani kuanzia mwanzo hadi mwisho, yaani Play back’, wakati mimi shabiki nimelipia kuona anachofanya jukwaani kiuhalisia, sio video shooting.
Cha ajabu kabla ya show utasikia ‘leo ntafanya kweli pale msikose’, ila nikifika nakuta naimbishwa na wimbo ule ule kama msanii anafanya video shooting, kufuatisha tu kile kilichoimbwa huku anafanya mbwembwe.
Huenda tunatofautiana nia na madhumuni ya kuhudhuria show ya msanii flani, mimi kwangu nia hua sio kumuona msanii, bali kumuona anatumbuiza kweli ule wimbo wake ninaokubali hadi nimeuweka kama mlio wa kuniamsha kwenda kazini, na mlio wa kupokelea simu.
Njia sahihi ya yeye kuperfom mimi simchagulii, lakini ni mwepesi wa kuona makosa ya wazi anayofanya ambayo kwa upande wangu naona hajanitendea haki. Pamoja na kukubaliana na yote na mbwembwe zinazofanyika jukwaani, sauti ya msanii husika kuimba kweli my favourite song pale jukwaani huwa ni kitu nachokipa priority.
Kama shabiki wa show, nimekuwa nikichukizwa na kitendo cha wasanii kuimba juu ya wimbo ‘play back’,mimi binafsi kwa kuwa naamini na naona kuna wengine tena wa level hiyo hiyo wanaimba Live, sio lazima iwe na band lakini angalau wameweka CD yenye beat kavu, ama beat chorus, au beat chorus na back vocal za studio. Hapo nafurahi, kuona energy ya msanii na kupata ladha mpya pale jukwaani.
Mi ni mmoja kati ya watu walioshuhudia performance ya rapper wa Tanzania ‘Webiro Wasira aka Wakazi kwenye Jukwaa la BBA 2013 kwenye Eviction, mwezi July na kuikubali sana show yake, aliimba kweli kama nilivyomuona pia Young Killer, Stamina, Weusi, Nikki Mbishi na wengine wakifanya hivyo.
Bahati nzuri nikakutana na Wakazi na hii ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana nae, sasa baada ya salaam ilibidi nimuombe muda tupige story kidogo kwa kuwa nilikuwa na kiu ya kutaka kujua na yeye kama msanii anachukuliaje swala la kupiga ‘Play Back’.
“Kusema ukweli navyoona unapokuwa unafanya kazi kama msanii lazima uoneshe reality na maturity kwamba umekuwa kisanii.” Wakazi alinambia.
Nilipigia mstari neno ‘reality’ kwa Kiswahili ‘Uhalisia’, na ndicho hicho nachokitaka kwenye show nazolipia mimi. Back vocal zinakuwepo kusapoti, lakini main ni kwake kweli.
Sasa hivi mimi naona baadhi ya wasanii wa Bongo wamejikita zaidi kutafuta dancers na kulipamba jukwaa na hao dancers, ni kweli wanafanya vizuri, lakini bado sioni kama ni sababu ya wao kuacha kuimba live kwa kuwa wana dancers na wanacheza pia, eti wanachoka sana! Kwangu mimi hainishawishi, mbona wapo wanaocheza na wanaimba pia, au wale wa bendi za dansi wao wanawezaje.
Ama kwa jinsi Young Killer anaweza kuweka pia break dancers na wao wakacheza wakati anaendelea kuimba hivyo hivyo, kama wakazi aliponda na wasichana waliopamba show wakati akikamua kweli.
Nilimuuliza pia Wakazi kuhusu hili, ili nipate wazo la msanii pia kwa sababu mimi ni kama mlalamikaji tu mwenye mantiki lakini.
“Maturity ni pale ambapo unakuwa unafanya mazoezi vizuri na umejidhatiti ili uwe na uwezo wa kucheza na kuimba, na uwe unajua wapi unapumzika na sehemu gani, kwa hiyo unaweza kucheza na ukaimba vilevile.” Wakazi alinipa hii.
Hapo nikapata wazo jingine, baadhi ya wasaniii wengi wa Tanzania tena wakubwa hunishangaza sometimes, pamoja na kutaja kiasi kikubwa cha pesa wanacholipwa kwenye shows, bado utaona wakialikwa sehemu kwenye show watakuja na crew ya watu sita au saba hivi, na kati ya hao utakuta wacheza show 4, na mpiga picha na mpambe wa ziada, hakuna Dj, mtu wa back vocal, mabaunsa wenye miwani mwieusi..! wala hawana muda wa kuajiri mweledi wa mambo ya kuhakikisha sauti zinatoka vizuri ( sound engineer). Hapo ni kama wanaandaa mazingira ya kushindwa kukwepa hiyo ‘Play Back’.
Hapo utasikia wanatoa vijisababu, utasikia amecheza sana hawezi kuimba Live, au vyombo havisikiki vizuri, mic sometimes zinakata sauti.
Hapo naona umuhimu wa kumtaja Profesa Jay na kumpa big up kwa kumtambulisha Dj Choka aliyekuwa Dj wa Choka Mbaya Crew, na pia mtu wake wa back vocal aliyekariri nyimbo nyingi za Profesa, na Dj Choka ameendelea kufanya kazi na wasanii wengine kama AY,Roma, Lady Jay Dee na wengine ambao kwa pamoja wamehakuwa wakihakikisha show zinaenda vizuri kama ‘Live show kweli’.
Nilipata pia mawazo ya Banana Zorro ambae ana uwezo mkubwa wa kuimba Live tena na Band, huku akipiga gitaa. Yeye aliongea kupitia The Chart ya 100.5 Times fm. Lakini yeye alinipa point nyingine tofauti kidogo na mtazamo wangu.
““Unajua kwa kawaida sio kwamba play back ni kitu kibaya, ama play back sio kwamba sio sanaa ama msanii akifanya play back hapaform, bali aina ya jinsi anavyofanya play back. Kwa sababu hata wasanii wakubwa wanafanya play back.”
Napata kigugumizi kidogo kuiga kila wanachofanya wasanii wakubwa wa nje kuwa kitakuwa sahihi, ndo nakumbuka mwalimu wangu wa chuo Mr. Sijjo alikuwa anasisitiza kuwa ‘dhambi ni dhambi’ tu hata kama akiifanya malaika itabaki kuwa dhambi.
Lakini point yake ya mfano wa baadhi ya wasanii wa bongo wanavyofanya inanishawishi kwa kuwa imekuwa funny lakini ina maana sana ya kile nilichokuwa nikikisema mimi.
“Sasa hivi unaangalia kuna show za Akon anafanya mchanganyiko play back, lakini aina gani, make sasa hivi kinachotokewa ni kwamba mtu leo akishasikia play back ndo dah..anaondoka na CD yake tena ile yenye cover ambayo inauzwa sokoni, anaenda kuiplay back sasa kwelikweli.”
Lakini kauli hii ya Banana Zorro kuwa hata wasanii wan je pia wanafanya play back, niliirudisha tena kwa wakazi kama swali, kutaka kufahamu yeye anadhani kwa nini hata hao wanaoitwa wakubwa wanaimba sometimes juu ya wimbo, na sometimes wanasimama kweli.
“Unajuwa kwa upande wa wasanii wakubwa unakuta anaamua kufanya hivyo kwa kuwa anakuwa na show 30 katika siku 20, kwa hiyo show nyingine anaweza asiipe umuhimu sana, kuona kama kuna umuhimu wa yeye kujionesha kuwa yuko katika kiwango flani, kwa hiyo akaamua tu kuwapa show ya kawaida, kwa kuwa anajuwa tu atashangiliwa, ni kitu kibaya kusema ukweli.”
Kumbe tatizo hapa inaweza kuwa ni uchaguzi wa umuhimu wa show, kwa ufupi inamaanisha kudharau baadhi ya show. Mi naona kama msanii amedharau pesa, ni vyema angedharau kile kiasi cha pes alicholipwa ili asije kwenye show mapema. Sio, kwenda kwenye show kutimiza tu ratiba.
Kama ulipata nafasi ya kuangalia ‘Coke Studio’, utaona jinsi ambavyo wasanii wa Afrika wana uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi kwa kuimba Live kama wale wa nchi za nje, ulimuona Diamond akiiua vilivyo ‘Temptetion ya P-Square’ , na Lady Jay Dee ambae ni kawaida yake kufanya na Live.
Hii inanisababisha nikubali kabisa kuwa wasanii wa kibongo wanaweza kufanya poa sana na kuachana na ‘Play back’.
Utajiuliza inakuwaje msanii anashindwa kuimba wimbo wake Live jukwani bila hiyo CD iliyoko radioni, wakati hata katika mashindano ya kuimba kama TPF6 na EBSS, washiriki wanaimba vizuri nyimbo za wasanii hawahawa wa bongo na wa nje, wanaziimba vizuri bila Play Back. Sasa inakuwaje mwenye wimbo mwenyewe ashindwe kuutendea haki jukwaani?
Hali hii inanifanya niungane na kauli ya Master J, jaji wa EBSS wakati akitoa maoni yake kwa baadhi ya washiriki wa EBSS.
“Narudia na ntaendelea kurudia sana hili, kuna watu wanaperform chini ya hapo huko nje, na wanamiliki magari na majumba.”
Sasa kwa mtindo huu nadhani huu ndio nauita ‘unyonyaji’ kwa kuwa msanii hufanya kazi chini ya kiwango japo anafanya vizuri kwa kiasi flani, na kwa kuwa mashabiki wengi hawajashitukia kudai haki yao, basi unakuwa ‘Unyonyaji uliohalalishwa’ kwa kupoozwa na neno ‘alishangiliwa sana, alifunika sana.
Wasanii wanaofanya hivyo kwa kisingizio chochote, na mnalipwa vizuri na mnatangaza, kumbukeni kauli ya Bob Marley, “You can fool all the people for sometimes, but you can’t fool all the people all the time.”
Badilika, fight for excellence, sio kwa mazoea na kuiga mfano wa aliyekosea hata kama ni msanii kutoka mwezini.
source:Josefly Muhozi