advert

http://

Monday, 16 September 2013

WALIOMBAKA MWANAFUNZI NDANI YA BASI WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA.



Wanaume wanne jana wamehukumiwa kifo kwa kuhusika na shambulio la ubakaji na mauaji ya msichana kwenye basi mjini Delhi. 
Jaji Yogesh Khanna, ambaye aliwatia hatiani wanaume hao kwa shambulio la ubakaji na 'kusababisha' mauaji mapema wiki hii, alikataa ombi la mwanasheria wao la kuwapunguzia adhabu wateja wake hao.
 

Shangwe zililipuka kutoka kwenye umati wa watu nje ya mahakama hiyo ya Delhi pale wanasheria walipotoka nje kwa kasi na kutangaza hukumu hiyo iliyotolewa kutokana na shambulio hilo la Desemba mwaka jana, ambalo liliibua maandamano makubwa kote nchini India na midahalo kadhaa kuhusu uhalifu dhidi ya wanawake.



"Hii imeshitua jamii nzima ya wapenda amani," Jaji Yogesh Khanna alisema, akiwahukumu wanaume hao adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
 
"Katika nyakati hizi huku uhalifu dhidi ya wanawake ukiongezeka, mahakama haziwezi kugeuka vipofu mbele ya makosa hayo ya kutisha."

Hukumu hiyo ilikuwa moja ya vipimo vikubwa kabisa kwa miaka kadhaa ya mtazamo wa kweli kinzani ya India kuelekea hukumu ya kifo.
 
Majaji wa nchini humo wanatoa, kwa wastani, hukumu 130 za kifo kila mwaka lakini India imeshaua watu watatu tu katika miaka 17 iliyopita.
 

Pichani ni nyuso za watu wanne walio hukumiwa adhabu ya kifo kwa ubakaji na mauaji ya kikatili ya  mwanamke kijana yaliya fanyika kwenye basi mjini New Delhi , Desemba mwaka jana.


Licha ya kusita kwake kutekeleza hukumu hizo, mwaka jana India ilipiga kura dhidi ya upitishwaji muswada wa Umoja wa Mataifa uliotaka ruhusa ya kusitishwa kwa muda adhabu za kifo.

Wanasheria wa watuhumiwa wote wanne walisema watakata rufani, kitu kinachomaanisha utekelezwaji hukumu zao unaweza kuwa miaka kadhaa ijayo. Kesi hii itakwenda katika Mahakama za Juu na kisha Mahakama Kuu.

Endapo zitathibitisha hukumu hizo, uamuzi wa mwisho utamtegemea Rais, ambaye ana mamlaka ya kufanya huruma.

Mmoja kati ya wanne hao, mwalimu wa gym Vinay Sharma, alimwaga machozi wakati akitolewa nje ya mahakama hiyo, ambako polisi wakiwa na vifaa vya kukabiliana na ghasia walijipanga kuzuia umati mkubwa wa wananchi.

Mwathirika huyo, ambaye alibakwa kwa saa moja na kujeruhiwa kwa nondo ndani ya basi lililokuwa kwenye mwendo, amekuwa alama ya hatari wanazokabiliwa nazo wanawake katika nchi ambayo ubakaji unaripotiwa kwa wastani wa kila dakika 21 na mashambulio ya tindikali na kesi za kukera yameshika kasi.

Mwanamke huyo, ambaye ametokea katika familia ya maisha ya kati na kufanya kazi kwenye kituo cha mawasiliano wakati akiwa anaendelea na masomo, hajatajwa kutokana na sababu za kisheria, lakini vyombo vya habari vya India vimempachika jina la Nirbhaya, neno la Kihindi linalomaanisha asiye na hofu.

"Leo tunaweza kupumua kidogo kirahisi," alisema mama wa mwathirika huyo, ambaye alimkumbatia ofisa mmoja wa polisi nje ya mahakama hiyo baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo. "Natumaini hukumu hiyo itawatisha watu kufanya makosa kama haya kwa siku za usoni."

Mawakili wa utetezi wameiasa mahakama hiyo kupuuza walichosema kimezagaa na shinikizo la kisiasa kutoa adhabu hiyo kali zaidi.

"Huu sio ushindi wa ukweli. Ila ni pigo kwa haki," wakili wa utetezi A.P. Singh aling'aka kwa jaji wakati hukumu hiyo ikisomwa.

"Jaji amechukua uamuzi huo chini ya shinikizo la kisiasa bila kujali uhalisia," aliwaeleza waandishi baadaye.

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo, Sushilkumar Shinde, alikanusha kwamba kulikuwa na muingilio wa kisiasa, akisema: "Hakuna mamlaka yoyote ya sheria inayoathiriwa na serikali.
"


 Mtoto EMILLY GEORGE[7] Mkazi wa kijiji cha RUANDA wilaya ya Mbeya akilia kwa uchungu maumivu ya vidonda baada ya kuchomwa moto na mama yake mzazi kisa akidaiwa kuiba mayai ya kuku jamani ukatili gani huu?
Wimbi la ukatili dhidi ya watoto bado limezidi kuchukua sura mpya baada ya mtoto EMILLY GEORGE[7] Mkazi wa kijiji cha RUANDA wilaya ya Mbeya kuunguzwa vibaya mikono yote miwili na mama yake mzazi ELESIA MWASILE[41] kwa maji ya moto kisha kufungiwa ndani kwa siku saba bila matibabu yoyote.

Akiongea huku akitetemeka kwa hofu ELESIA amesema kuwa chanzo cha cha kumchoma mtoto huyo ni kutokana na malalamiko ya majirani wakimtuhumu mtoto huyo kujihusisha na vitendo vya wizi vikiwemo wizi wa pesa na mayai ya kuku.

Tukio la mwisho lililopelekea mtoto huyo hadi kuchomwa ni pale ilipodaiwa na mama huyo kuwa mtoto aliiba mayai akidai amechoshwa na tabia za malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa jirani zake.

Baada ya kuunguzwa kikatili mtoto huyo alifungiwa ndani kwa siku saba bila matibabu yoyote hali iliyowafanya majirani kuuliza aliko mtoto kutokana na mtoto huyo kutoonekana mitaani hali iliyopelekea kutolewa taarifa ofisi ya kijiji ili kubaini aliko mtoto.

Uongozi wa kijiji baada ya kupata taarifa kwa majirani walifanya upekuzi na kumkuta mtoto amefungiwa ndani huku akiwa na majeraha makubwa katika mikono yote miwili ndipo taarifa ilitolewa kituo cha Polisi MBALIZI ambapo mama huyo alikamatwa.

Baada ya kukamatwa mama huyo katili alkabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya D\SSGT PUDENSIANA BAITU na Mwenyekiti MARY GUMBO ambaye muda wote alikuwa akiangua kilio kutokana na kitendo alichofanyiwa mtoto na mama yake mzazi.

Hivi sasa mwanamke huyo anahojiwa na Polisi kituo kikuu cha kati na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo na mtoto amelazwa katika Hospitali ya Rufaa wadi namba tano akiendelea kupatiwa matibabu.

Vitendo vya unyanyasaji vimendelea kukemewa Mkoani Mbeya na Asasi mbalimbali hasa kwa watoto vikiwemo vya ubakwaji,ulawiti,kazi za ndani na baadhi ya watoto wamepata ulemavu wa kudumu ikiwemo kupoteza viungo.
 Mama mzazi wa mtoto aliyechomwa moto ELESIA MWASILE[41] akipelekwa kituoni na wanausalama
Hapa wanausalama na mama mzazi wa mtoto huyo wakielekea kumwona mtoto huyo katika hospitali ya Rufaa Mbeya

Baada ya kukamatwa mama huyo katili alikabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya D\SSGT PUDENSIANA BAITU akimjulia hali mtoto Emilly

Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana, imebainika kuwa alitishiwa kuuawa miezi mitatu kabla ya kukutwa na tukio hilo. 

Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Dk Shein alisema Polisi inatakiwa kuongeza nguvu za uchunguzi ili kukabiliana na matukio ya kikatili ya umwagaji wa tindikali, yanayoshamili visiwani humo hivi sasa.
“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee … ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Dk Shein.
Dk Sheni alisema, kitendo hicho ni cha kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo.
Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
“Unajua kawaida ya watu wa Zanzibar hufanya mazoezi barabarani, sasa kipindi anapita eneo hilo katika kilima, kuna mtu alimwambia atamfanyia kitu kibaya ambacho hatujui ndiyo hiki au la,” alisema Padri Assenga na kuongeza:
Alisema Juni mwaka huu mara baada ya kupewa vitisho hivyo alikwenda kutoa taarifa kwa Sheha wa eneo hilo na kituo cha polisi.
“Mara baada ya kutolewa vitisho hivyo Juni mwaka huu, alichukua jukumu la kwenda kutoa taarifa kwa mkuu wa eneo hilo (Sheha) na kituo cha polisi.”
Akielezea tukio la kumwagiwa tindikali Padri Mwang’amba, alisema alimwagiwa saa 9:45 alasiri juzi wakati akizungumza na simu nje ya internet cafĂ© iliyopo eneo la Mlandege.

Waziri wa uchukuzi Dkt. Harrisoni Mwakyembe amebaini wizi wa mafuta katika bomba la mafuta mjimwema na kuagiza maskari wa usimamizi wa bandari Tanzania kuwakilisha majina ya wahusika ndani ya siku mbili.


Mwakyembe ameyasema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) na kulaani kitendo cha baadhi ya watu kutoboa bomba hilo na kuunganishia mabomba yao madogo na kuyafungia kwenye maputo yenye uwezo wa kubeba mafuta kati ya lita 16-18 kinyume cha sheria na kukiita kitendo hicho ni kuhujumu uchumi wa nchi ambapo ameishutumu kampani ya ulinzi ya tipa kuhusika na kitendo hicho na kuwataka kumpa picha za wafanyakazi wote waliokuwa kitengo cha ulinzi na kama hawatafanya hivyo kampuni hiyo italipishwa fidia.

Naye kaimu mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania Mhandisi Madeni Kipande wakati akijibu mapendekezo yaliyotolewa na waziri mwakyembe kuhusu wafanyakazi wa mamalaka hiyo amesema kuwa wafanyakazi waliokuwa wameajiriwa kama vibarua watapewa ajira za kudumu na kubainisha kuongezewa posho wafanyakazi hao kutoka laki moja awali na kufikia laki mbili pamoja na laki moja na nusu kama ghrama za chakula


SOURCE-ITV. 

Afya za Watanzania ziko shakani kutokana na kuwapo kwa biashara ya kuingiza samaki kutoka nje ya nchi, wanaodaiwa kuharibika na kuuzwa katika la Soko la Feri jijini Dar es Salaam.


Samaki hao kutoka Yemen, Dubai, China na Japan, wanaoingizwa nchini wakiwa wameganda kwenye barafu, wengi huharibika muda mfupi baada ya barafu kuyeyuka au baada ya kununuliwa.

Uchunguzi umegundua kuwa samaki hao huletwa nchini kutafutiwa soko baada ya kukaa kwenye majokofu kwa muda mrefu huko wanakotoka, kiasi cha kuelekea kuharibika.

Ili wasiharibike, samaki hao aina ya Marckerel hukaangwa hadi wakauke. Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wanunuzi wake wakuu ni wafanyabiashara wa chakula wakiwamo wamiliki wa migahawa na Mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika miji ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma.

Samaki hao wanauzwa kwa bei ya chini ambayo ni Sh38,000 kwa boksi lenye uzito wa kilo 15, ikilinganishwa na wanaovuliwa hapa nchini ambao bei yake ni Sh60,000, kwa uzito huohuo.

Inaelezwa kuwa samaki hao baadhi yake ni wale ambao wamekwisha muda wake wa kutumika katika nchi hizo, hivyo kuingizwa nchini kutafutiwa soko.

Dk Raymond Mwenekano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anayataja madhara ya ulaji wa samaki wa aina hiyo kuwa ni kupata magonjwa kama vile kansa ya utumbo, mwili kuwasha, kubabuka na vidonda mwilini.

“Madhara yake ni makubwa, ndiyo maana siku zote tunasisitiza kula vyakula visivyokaa sana kwani vingine vimehifadhiwa kwa dawa na wanaofanya hivi ni wafanyabiashara kwa faida yao,” alisema Dk Mwenekano.