Hukumu ya muimbaji Nguza Viking aka Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza aka Papii Kocha imepangwa kupitiwa tena October 30 mwaka huu na majaji watatu wa Mahakama ya rufaa nchini.
Babu Seya na Papii Kocha wanaendelea kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kukutwa na hatia kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto wadogo. Hukumu hiyo ilitolewa Februari, mwaka 2010 na Jopo la majaji wakiongozwa na Natharia Kimaro.
Watoto wawili wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis Nguza waliachiwa baada ya kubainika hawana hatia kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto. Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani, mapitio ya hukumu hiyo yatasikilizwa Oktoba 30, mwaka huu na majaji hao watatu waliotoa hukumu ya rufaa.
Babu Seya na mwanaye Papii Kocha, Mbangu na Francis walihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2004 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Katika hukumu hiyo ya Juni 25, 2004, Hakimu Mkazi Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanawe watatu kwa makosa 23 ya ubakaji na ulawiti na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Baada ya kupewa adhabu hiyo, Babu Seya na wanaye walikata rufani Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ambapo Jaji Thomas Mihayo (mstaafu kwa sasa), aliwatia hatiani na kuunga mkono hukumu ya Mahakama ya Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Lyamuya.
Kutokana na hukumu ya Mahakama Kuu, Babu Seya na wanaye waliamua kwenda Mahakama ya Rufani, ambako Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walitiwa hatiani wakati Mbangu na Francis waliachiwa huru.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo , Mahakama iliridhika na ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo kwa kila kosa na kwamba mrufani wa kwanza (Babu Seya) na wa pili (Papii Kocha), walihusika katika kutenda makosa. Ilisema utetezi wao kuwa hawakuwepo katika eneo la tukio ulikataliwa.
Katika hukumu hiyo, Babu Seya alitiwa hatiani kwa makosa matano ya kubaka na Papii Kocha alitiwa hatiani kwa makosa mawili.
Chanzo: Habari Leo
|
Bango/Billiboard linaloonesha picha ya Yesu ikiwa imechorwa tattoo imewakasirisha wakristo waishio Texas Marekani, hasa West Lubbock ambako ndiko bango hilo lilipowekwa.
Mkazi mmoja wa eneo hilo alipoulizwa alisema, “siipendi hiyo picha, naona kama inaonesha dharau/inadhalilisha.”Mwingine alisema, “mininafikiri inakufuru.”
Bango hilo linaonesha picha inayotumika sana kuashirika taswira ya Yesu Kristo, zinaomuonesha akiwa amevaa taji la miiba huku akiwa amechorwa tattoo zilizoandikwa dhambi za wote walienda kwake na akawasamehe, hivyo wachoraji wanaashiria amebaki nazo na wao wako safi!
Hata hivyo ,kundi la watu ambao wameweka bango hilo wamelitetea na kudai kwamba wamechora na kuliweka kwa nia nzuri ili kuwahubiri watu waende kwake na kusafishwa dhambi zao.
Bango hilo limeandikwa address ya tovuti ambayo ina video inayoonesha watu wanaenda kwa Yesu na wanasafishwa dhambi zao.
|
Kwa kawaida msanii anapotoka na kuhit sana huombwa kushirikishwa kwenye nyimbo za wasanii wenzake nyingi na tumekuwa tukiona baadhi ya wasanii wakidiriki kusema wamesitisha kufanya collabo na wasanii ama wanahitaji kulipwa kiasi flani cha pesa na anaetaka kuwashirikisha.
Hii ni tofauti kwa mkali wa michano yenye style yenye ladha ya Kaskazini Janjaro, ambae pamoja na kuwa na hits nyingi hewani na kupiga show hadi Afrika Kusini, ameshawahi kushirikishwa kwenye wimbo mmoja tu tangu aanze muziki, I mean tangu akiwa Arusha wakati hajaingia kwenye mkondo mkubwa wa Muziki TZ (Main stream).
“Nilishawahi kushirikishwa kwenye wimbo mmoja tu unaoitwa ‘Shikamoo Mwalimu’, nilifanya na Easy Muchwa, ma-producer walioufanya ni P-Funk Majani na Chizan Brain, ile ya Madee (Nisikilize) nilifanya intro tu na sikuandikwa kama nimeshirikishwa. Nilipokuwa Arusha nilifanya nyimbo zangu tu lakini sikushirikishwa.” Janjaro ameiambia tovuti ya Times Fm.
Wimbo aliofanya na Asley(Nimeshamaliza) ulikuwa wimbo wao wa pamoja. Janjaro ameshawashirikisha wasanii kadhaa kwenye project zake akiwemo Tunda Man, Chege, Godzilla, PNC, Jambo Squared na wengine.
Hata hivyo Janjaro atakuwa kwenye Project kubwa ya Dj Choka itakayowashirikisha wasanii wenye umri mdogo, na waliotajwa kushiriki ni pamoja na Young Dee, Country Boy na M-Rap. Project hiyo inafanyika katika studio za BHitz chini ya producer Pancho.
Huu ndio wimbo pekee aliowahi kushirikishwa officially Janjaro:
|
Ingawa mara nyingi husemwa kuwa hakuna usalama wa asilimia mia moja kwenye ulimwengu wa teknolojia ya kompyuta, ila kinga ni bora kuliko tiba.
Umewahi kujiuliza kwa nini watu wengi wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ya makazi?
Ndivyo ilivyo, tembelea hata katika makazi ya watu wa kawaida, madirisha yamejaa nondo, nyumba zimezungukwa na kuta ndefundefu. Wengine wamefikia hatua ya kufuga mbwa kwa ajili ya kuwalinda.
Nimeanza kwa kutoa mifano hii kuonyesha umuhimu wa kuzilinda kompyuta zetu. Ingawa mara nyingi husikika ikisemwa kuwa hakuna usalama wa asilimia mia moja kwenye ulimwengu wa teknolojia ya kompyuta, ila kinga ni bora kuliko tiba.
Cha msingi ni kufuata tu kanuni, kwani kwa kufanya hivyo unaweza kwa kiasi kikubwa kuepukana na mambo mengi yanayoweza kuhatarisha usalama wa kompyuta yako kama vile athari za virusi.
Makala haya yanataja baadhi ya kanuni za msingi unazopaswa kufuata ili kutunza usalama wa kompyuta yako.
Tumia programu unazozihitaji
Watumiaji wengi wa kompyuta tumekuwa waathirika wa matatizo ya kompyuta zetu ama kwa kujua au kwa kutokujua. Kwanza ieleweke kuwa kompyuta nyingi zimekuwa zikiathiriwa kiusalama kwa makosa yaliyomo kwenye kompyuta husika.
Hizi ni zile kompyuta zenye programu ambazo hazijaandikwa kiusahihi. Tuchukue mfano wa nyumba inayovuja, kwa kuwa tu paa lake halikuezekwa ipasavyo. Au ukuta wa nyumba unavyoweza kuanguka, kwa kuwa haukutengenezwa kwa kufuata taratibu za ujenzi.
Kama kompyuta yako ina programu ambayo haikuandikwa kwa usahihi, matatizo mengi hutokea yanayoweza kuhatarisha kifaa hicho. Programu hizi sio tu zitahitilafiana na mtambo endeshi (OS) wa kompyuta yako, pia zinaweza kutoa mianya kwa wavamizi kuingia kwenye kompyuta yako kupitia kwenye mianya iliyopo kwenye programu hizi.
Cha kufanya: Mosi, ondoa programu usizotumia. Tuache tabia ya kuweka programu nyingi katika kompyuta zetu ambazo kwa hali ilivyo hatuzitumii kabisa. Kwa kawaida programu hujaza nafasi, kuweka uchafu na hatimaye kuiweka kompyuta matatani.
Kumbuka unapoweka (install) baadhi ya programu katika kompyuta yako, nazo huweka programu nyingine zinazoambatana nazo bila ya wewe kujua. Hatimaye unajikuta umelundika lundo la programu.
Tuangalie mfano huu; unapoweka programu ya Microsoft office, tafiti zinaonyesha watumiaji wengi hutumia programu kubwa tatu ambazo ni Word, Excel na Power Point.
Ieleweke kwenye kila bunda la programu ya Microsoft kuna programu nyingine zaidi ya kumi ndani yake ambazo zote huwekwa pamoja, lakini hazitumiwi kabisa au zinatumiwa mara chache mno.
Wataalamu wanashauri tunapotaka kuweka programu tuchague kile kwa kuzingatia kile kinachojulikana kama ‘custom Installation’. Uwekaji wa aina hii siyo tu unaweza kukuelekeza wapi uweke programu, bali pia utaweza kuchagua aina ya programu unazotaka kuweka kwenye kompyuta yako.
Pili, hakikisha unatumia programu zinazokwenda na wakati. Fanya uboreshaji wa matoleo mapya ya programu unazotumia (update)unapohitajika. Tuache hofu ya kutumia uboreshaji kwa hofu ya kufutiwa usajili wa programu au labda yataathiri kompyuta yako.
Cha muhimu kuzingatia ni kuwa kila yanapotoka matoleo mapya, wahusika wanalenga kutusaidia watumiaji na siyo vinginevyo.
Hakikisha unatumia programu halisi au kuichukua moja kwa moja kutoka kwenye wavuti ya watengenezaji au sehemu salama kama ilivyoelekezwa na mtengenezaji.
Kuwa na programu halisi sio tu itaiwezesha kompyuta yako kuwa imara, bali pia itakuwezesha kupata maboresho pindi yanapotoka kama tulivyoelezea hapo juu. Kiuhalisia, programu nyingi bandia (siyo zote) huvunja mfumo asili wa programu na kuifanya iwe dhahifu, huku nyingine zikipandikiza minyoo kwa mtindo wa viraka (patch) inayokwenda kuharibu mwendendo wa programu halisi.
Kwa mtindo huu unarahisisha kifaa chako kushambuliwa. Hivyo, matumizi ya programu bandia hasa kwa mitambo endeshi ni hatari kwa usalama wako.
Leo hii katika baadhi ya ofisi, wataalamu wa Tehama huweka mitambo endeshi bandia bila uongozi kufahamu, hivyo kuiweka kampuni kwenye hatari ya uvamizi.
Ushauri kwa wenye kampuni, wahakikishe wanatafuta Mkaguzi wa Tehama (IT Auditor) afanyie tathmini ya vifaa vyote ili kubaini dosari kama hizi.
Tumia programu za uhakika.
Umewahi kujiuliza kwanini natumia programu hii badala ya ile? Ukuaji wa teknolojia umesababisha kila mtu kuja na programu yake. Kwa mfano, kuna zinazotolewa bure au zinazouzwa kwa bei ya chini. Kumbuka, programu ya uhakika siyo lazima iwe inauzwa, kuna programu nyingi zinauzwa kwa bei ya juu, lakini zimekuwa na matatizo mengi kuliko zinazotolewa bure.
Kuhusu programu zinazotolewa bure, siyo kama hazina ubora, natoa rai kwa watumiaji kufanya utafiti kabla ya kuamua kutumia programu fulani.
Tena siku hizi ‘mtandao wa google’ unaweza kukusaidia kwa kiasi kikubwa kufanya utafiti na hata kujua maoni ya watumiaji wa programu husika.
Nitoe mfano dhahiri. Niliwahi kutumia Windows XP siku za nyuma. Nilipotaka kubadilisha mtambo, nikagundua watu wengi walikuwa wakilalamika kuhusu Windows Vista.
Baada ya kufanya utafiti nami nikabaini kuwa Windows Vista ingenisumbua, hivyo nilighairi kuitumia ingawa ilikuwa na mwonekano mzuri. Jambo la kushukuru ni kwamba kampuni husika (Microsoft) nayo ilibaini tatizo hivyo ikaiondoa Windows Vista sokoni na kuingiza Windows 7 ambayo imekuwa ikipendwa na watumiaji wengi.
Utafiti wangu unaonyesha watumiaji wengi wa kompyuta tumekuwa waathirika kutokana na kukubali kiholela au kufanya mambo tusiyoyajua.
Nitoe mfano kuhusu hili. Jamaa yangu wa karibu aliwahi kuvamiwa na programu za matangazo (adware).Alipofungua tovuti fulani akakumbana na tangazo lililomwelekeza kubonyeza mahala fulani kwa kuwa tangazo lilimwambia kompyuta yake ilikuwa katika hatari.
Bila kujua anachokifanya akabofya na kujikuta ameshaingiza madudu kibao katika kompyuta yake. Hivyo kuwa makini kila unapokabili ujumbe wowote. Hakikisha unasoma na unajua unachokifanya na wala si kubonyezabonyeza.
Haya ni mambo machache unayotakiwa kuzingatia ili kuhakikisha kompyuta yako iko katika mazingira salama na yenye kinga.
Mwananchi.
|
Kama umeshushwa thamani unakuwa kwenye hatari ya kuachwa. Hata kama mwenzako alikuwa ameshafikiria suala la kuingia kwenye ndoa na wewe lakini kwa sababu ameshakushusha thamani ndoa inaweza kuyeyuka.
Ukiwa kwenye ndoa ni hatari zaidi maana mwenzako hukuchukulia wa kawaida – mazoea huzidi na hapo ndipo uhitaji wa kuwa na mwingine wa pembeni unapoanzia. Haoni cha muhimu tena kwako, ndiyo maana wazo hilo huvamia ubongo wake kwa kasi sana.
Itafikia hatua, kama upo ndani ya ndoa, mwenzako atagoma kuongozana na wewe na kama ikitokea hivyo mkikutana na rafiki zake njiani hatakutambulisha. Hisia kwamba hamuendani humwingia.
UNAFANYAJE SASA?
Kubwa unalotakiwa kufahamu rafiki yangu mpendwa, suala la kupanda au kushuka thamani lipo mikononi mwako. Yapo mambo ambayo ukiyazingatia, mwenzako hawezi kukuchoka na kufikia hatua ya kukushusha thamani.
Tayari tumeshaona athari zake lakini hapa sasa nataka kukupa mbinu ambazo ukiwa nazo makini basi itakuwa rahisi kwako kubaki namba moja na mtu muhimu zaidi (ndiyo inavyotakiwa kuwa) kwa mpenzi wako maana ni haki yako.
ANZIA MWANZO
Ni rahisi zaidi kulinda thamani yako kuanzia mwanzo wa uhusiano wenu. Ikiwa tayari mmeshakomaa halafu tatizo hilo likajitokeza, hutumika nguvu nyingi zaidi kulirekebisha kuliko kujizatiti kuanzia mwanzo wa uhusiano. Ni mambo gani hayo? Twende hapo chini.
CHUNGA KAULI ZAKO
Naomba ieleweke wazi kuwa mada hii ni maalum zaidi kwa wanawake. Kitu muhimu cha kwanza kabisa kwa mwanamke ambaye anataka kuilinda thamani yake kwa mpenziwe ni kupima sana kauli zake.
Acha kuropoka hovyo, pima maneno yako na ikiwezekana kama unadhani kuna jambo huna uhakika nalo usizungumze kabisa. Katika eneo hili, uwe makini zaidi mnapokuwa na watu wengine. Kama mwanamke usiwe mchangiaji hoja sana.
Utulivu wako unaweza kuwa silaha kubwa ya kukufanya ubaki na thamani yako kama mwanamke anayejitambua.
USIRUHUSU MAPENZI
Msichana mwenye kujitambua na kufahamu thamani yake sawasawa hawezi kuruhusu mwili wake ujulikane na mwanaume harakaharaka. Onesha unajitambua na usikubali kirahisi kuuacha mwili wako uchezewe.
Mpe hoja; kwanza mapema, hajakuoa wala kukuchumbia, haraka ya nini? Wakati unawaza kuhusu kutoa penzi lako, lazima ufikirie kuhusu athari zinazoweza kukupata kwa kukurupukia mapenzi. Mwanaume ambaye bado hamjachunguzana na huna uhakika naye wa kutengeneza maisha, kichwani mwake hakuweki kwa asilimia kubwa.
Ukumbuke kwamba, ukipata matatizo yoyote – binafsi au yanayosababishwa na uhusiano wenu, anakuwa hana uwajibikaji wa asilimia kubwa kwa tatizo hilo. Utabaki wewe na matatizo yako!
|
Rais Jakaya Kikwete amesema maadui wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka kuvuruga nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo na upepo mbaya, lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni, maadui wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi, lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na nchi iko salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania itasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu. Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa mchakato wa kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja umoja wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.
-Mwananchi
|
Hali ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro aliyejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi mbili juzi huko Kibamba, Dar es Salaam inazidi kuimarika na jana alizungumza na gazeti hili na kusema; “Sijambo, naendelea vizuri.”
Ufoo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hata hivyo, anazungumza kwa shida kutokana na kukabiliwa na maumivu baada ya kufanyiwa upasuaji juzi.
Mwandishi huyo amehamishiwa katika wodi ya upasuaji wa moyo huku kiongozi wa wodi hiyo, ambaye alikataa jina lake kuandikwa gazetini, akieleza kuwa walimhamishia huko ili apate muda zaidi wa kupumzika.
“Watu wanakuja kwa wingi kumjulia hali, tuliona tumhamishe ili apumzike,” alisema kiongozi huyo.
Kabla ya kupelekwa katika wodi hiyo, Ufoo alikuwa katika wodi ya Kibasila na baadaye alihamishiwa katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Ufoo alipigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua baadaye. Pia Mushi anatuhumiwa kumuua mama yake Ufoo, Anastazia Saro wakati wa tukio hilo.
Mazishi ya mama yake Ufoo yamepangwa kufanyika Ijumaa huko Machame mkoani Kilimanjaro.
Ufoo aongea kwa shida
Mara baada ya mwandishi wa gazeti hili jana kuingia
katika chumba alicholazwa Ufoo huku akisindikizwa na wauguzi watatu, mwandishi huyo alitoa mkono wake na kusema; “Njoo hapa unisalimie huku umenishika mkono.”
Huku akionyesha uchovu na kusikia maumivu, alizungumza kwa tabu na kusema; “Sijambo naendelea vizuri.”
Mara baada ya wauguzi hao kumweleza kuwa kati ya waandishi zaidi ya 30 waliofika kumjulia hali ni watatu tu ndiyo walioruhusiwa kumwona alitaka kujua ni kina nani waliobaki nje kwa kuhoji; “Nani hao wako nje.”
-Mwananchi
|
Msemaji wa DMX 'Domenick Nati' amesema rapper huyo na Swizz Beatz wameanza kufanya kazi pamoja kwenye album mpya ya Dog Man X ila mpaka sasa hatujajua lini cd hio inatoka. Swizz Beats na Dmx wameonekana pamoja miezi michache iliyopita kwenye tamasha la Alicia Keys.
Fahamu kuwa rapper Dmx amekuwa akikabiliwa na matatizo ya kisheria pamoja na kuishiwa. Hivi karibuni alimwambia mtangazaji moja huko Marekani kuwa amebakiwa na dolla 50 tu kwenye account yake ya benki so huu utakuwa mpango mzuri wa kumrudisha tena juu rapper huyu.
|
KITENDO cha kudaiwa kugoma kuhama nyumba anayoishi mtangazaji wa Independent Television (ITV) na Radio One, Ufoo Peter Saro iliyopo Mbezi, Dar kinadaiwa ndiyo chanzo cha kupigwa risasi na kujeruhiwa na mchumba’ake, Anther Mushi ambaye naye alijiua.
Akizungumza na Uwazi, juzi nyumbani kwao Kibamba Dar, mdogo wa Ufoo aitwaye Goodluck Saro alisema ugomvi anaoujua yeye ni kitendo cha dada yake huyo kukataa kuhamia kwenye nyumba ya Kimara, Dar ambayo Anther aliipanga.
Alisema hajui kwa undani ni kwa nini dada yake alikuwa akigoma kuhamia makazi hayo mapya lakini kitendo hicho kilikuwa kikimfanya shemeji yake kubadilika. “Siku za hivi karibuni shemeji alibadilika hata tabia. Zamani alikuwa akija anatuchangamkia sana, siku za hivi karibuni alikuwa akija, baada ya salamu haongei,” alisema Goodluck.
Wakizungumza na gazeti hili juzi, saa chache baada ya tukio hilo, baadhi ya majirani wa nyumbani kwa akina Ufoo walisema walishtushwa na milio ya risasi kutoka kwenye nyumba ya mama Ufoo, Anastazia Peter Saro wakidhani amevamiwa na majambazi. “Ilikuwa saa kumi na moja alfajiri, mimi nilikuwa nimeshtuka kutoka usingizini lakini sijatoka kitandani, nilisikia milio ya risasi, nilijua mama Ufoo amevamiwa na majambazi. “Lakini nikiwa najipanga jinsi ya kutoka nikasikia sauti ya mama Ufoo akisema jamani nakufa huku Ufoo akipiga kelele za kuomba msaada, nikashangaa maana najua haishi hapo, kwenda nikamuona Ufoo yupo nje akikimbia hovyo na damu chapachapa maeneo ya kifuani na mgongoni. “Nilimuuliza kuna nini, kabla hajanijibu nikamwona mwanaume wake anatoka nje akiwa peku. Akasimama na kupiga risasi nyingine hewani kisha akaingia ndani. “Muda huohuo nikasikia mlio mwingine wa risasi, nikajua kuna mauaji makubwa sana,” alisema jirani huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake. Jirani mwingine alisema alishtushwa sana na milio ya risasi, akaminya ndani akijua ni majambazi mpaka baadaye aliposikia watu wakilia huku wakisema mama Ufoo ameuawa kwa risasi na mkwe wake. Habari nyingine zinadai kuwa Anther kabla ya kujiua, alikaa kwenye kochi kwanza na kujiandaa ambapo alisema: “Nimezaliwa siku moja nitakufa siku moja.” Akajilipua! Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, marehemu Anther alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan. Habari za ndani zinadai kuwa usiku wa kuamkia siku ya tukio, mwanaume huyo akiwa nyumbani kwa Ufoo, Mbezi, Dar hawakulala kwa ugomvi ambapo marehemu alisikika akimshutumu mchumba wake huyo mambo ambayo hakuyaweka wazi. Ikadaiwa kuwa ili kumaliza mgogoro, saa kumi na nusu alfajiri waliondoka kwenda Kibamba kwa mama wa Ufoo ili akasaidie kurejesha amani. Katika kurudisha amani, mama Ufoo alikuwa mstari wa katikati, akiwa hapendelei lakini marehemu Anther alimshutumu mama mkwe wake huyo kwamba anampendelea mwanaye. Ndipo alipotoa bastola na kuielekeza kwa mama Ufoo na kumpiga risasi ya kifuani. Mama huyo alianguka na kukata roho papo hapo. Aliielekeza bastola kwa Ufoo na kumfyatulia risasi nne, mbili kifuani, moja begani na nyingine tumboni ambapo damu zilimtoka kwa wingi.
Ufoo alikimbizwa katika Hospitali Teule ya Tumbi (Kibaha) na baadaye kukimbizwa Muhimbili.
GPL.
|
Mchungaji wa Kanisa la GRC, Anthony Lusekelo ‘ Mzee wa Upako’ amesema hatatoa ng’o fedha za rambirambi za Askofu Moses Kulola kutokana na kudhalilishwa kulikofanywa na wahusika wa kukusanya fedha hizo. Mzee wa Upako alisema badala yake fedha hizo shilingi milioni 15 sasa zitatumika kutibu maumivu aliyoyapata kutokana na vyombo vya habari kuandika utata juu ya ahadi yake ya kutoa rambirambi hizo.
“Kwanza mimi mtu aliyetajwa kuwa angekusanya fedha hizo ambaye ni Mweka Hazina wa Kanisa la EAGT, Mchungaji Praygod Mgonja simjui kwa sura, nilishamueleza njia gani muafaka ya uwasilishaji wa fedha hizo, badala yake akatumia vyombo vya habari kunidhalilisha.
“Nilimwambia Mchungaji Mgonja kuwa shilingi milioni kumi na tano siyo kama shilingi laki tatu; Zinapaswa kuwa na utaratibu unaoeleweka wa kutolewa. Nikamwambia mama Kulola (mke wa marehemu) azifuate mwenyewe ili aniombee baraka, akasema sawa, sasa nashangaa ananidhalilisha,” alisema Mzee wa Upako.
Alisisitiza kauli yake hiyo pia kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno wa simu kwa mwandishi wa habari hii kuwa hatatoa ng’o fungu lake aliloliahidi.
Aliongeza kuwa kwa sasa ameghairi kutoa fedha hizo kwa kuwa anadhani kuna njama fulani ambazo hakuzitaja na kwamba fedha hizo sasa atazitumia kutibu majeraha aliyoyapata baada ya habari kutoka katika vyombo vya habari.
Mchungaji Mgonja alisema kuwa hajapokea rambirambi za Mzee wa Upako ambazo ni shilingi milioni 15 na wengine walioahidi akiwemo Mchungaji Josephat Gwajima aliyeahidi kutoa shilingi milioni 10 na Mchungaji Getrude Lwakatare (shilingi milioni moja) walishatoa.
|
Nay wa Mitego anahisi maisha yake yapo hatarini kwa sasa baada ya vitisho kutoka kwa watu mbalimbali kuendelea kumwandama.
Rapper huyo wa Salam Zao, ameshare taarifa hizo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
“Huu muziki sasa utanitoa roho..!! sinaga ugomvi na mtu lakini kumbe kuna watu wanachuki serious na wanatamani atanife leo au wanitoe roho..!! Mi nafanya muziki vita yenu juu yangu namuachia mungu#966 mi nafanya kazi nzuri..! Hakuna wakunirudisha nyuma,, logeni niwindeni kwa vyovyote mtafeli 2. Mi siko wakawaida kiivyo itakula kwenu,” aliandika.
Baada ya kauli hiyo Bongo5 ilimtafuta Nay, ambaye alisema kuwa muziki ni sehemu ya maisha yake na wala hataogopa chochote wala kusita kufanya kile anachoona astahili kukifanya.
“Nimeshaona jinsi gani muziki unaniongezea maadui nashangaa hata watu ambao sina ugomvi nao wana chuki na mimi na wapo tayari kunifanya chochote,” aliongeza.
-Bongo5
|
Akizungumza na DJ HAAZU katika kipindi cha Dundo cha MJ RADIO Arusha, Noorah ambaye hivi karibuni alifunga pingu za maisha, alisema muziki hauna faida kwake na kwa sasa anaufanya kama starehe tu.
“Maisha ni malengo, kitu hata kama unaweza vipi, hata kama watu wanakupenda vipi kwenye hicho kitu, kama hakina manufaa mazuri kwako, hakina maana kwako,” alisema Noorah.
“Mimi muziki kama naufanya, naufanya kwa starehe zangu tu, haya mambo ya kutoa single, ifanye hivi, biashara hiyo sasa hivi haipo kwangu.”
Noorah aliongeza kuwa muziki wa Tanzania una siasa nyingi kiasi ambacho hata wale wanaonekana wamefanikiwa hawana lolote.
|