G8 Tanzania na Ukwepaji Kodi
Wakati dunia nzima ipo kwenye kampeni kubwa dhidi ya ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni kubwa duniani zinazowekeza kwenye nchi zinazoendelea, Tanzania ipo kimya kabisa kana kwamba hakuna linalotokea. Licha ya kwamba Bunge la Tanzania ni Bunge la Kwanza katika nchi za SADC kupitisha Azimio kuchunguza utoroshwaji wa Fedha (Azimio la Bunge namba 9/2012), Serikali ya Tanzania imekaa kimya kabisa kupaza sauti yake kuhusu ukwepaji kodi mkubwa.
Tanzania inapoteza mapato ya ndani sawa na asilimia tano (5) ya Pato la Taifa kupitia kodi za kimataifa ambayo ni sawa na shilingi trilioni mbili kila mwaka. Uchunguzi unaonyesha kwamba katika orodha ya walipa kodi wakubwa 10, kampuni saba zinatumia ‘tax havens’ kukwepa kodi. Katika kampuni kubwa tatu za simu hapa nchini kampuni mbili zimesajiliwa ‘tax havens’ za Uholanzi na Luxembourg na hivyo kukwepa kodi mbalimbali hapa nchini. Kampuni moja kubwa ya madini hapa nchini ina kampuni dada tisa (9) katika offshore hali kadhalika kampuni moja kubwa ya kutafuta mafuta na gesi hapa nchini. Katika mahojiano na gazeti la Financial Times la Uingereza la mwezi June, 2013 kampuni ya African Barrick Gold imetangaza kufunga baadhi ya kampuni zaidi ya 24 iliyoyasajili maeneo kama Cayman Islands.
Mheshimiwa Spika, bila Serikali ya Tanzania kuamua kwa dhati kusafisha nyumba yake, hata juhudi kubwa zinazofanywa na asasi za kiraia kama Oxfam, ActionAid, Tax Justice Network nk katika kupambana na ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha hazitafua dafu. Wakati nchi za G8 zinaweka mipango ya kutusaidia na sisi kama nchi tuweke mipango yetu wenyewe. Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza hatua za awali zifuatazo zichukuliwe ili kukabiliana na utoroshaji mkubwa wa fedha unaotokana na ukwepaji wa kodi;
(i) Tanzania ijiondoe kabisa katika mfumo wa kodi unaopendekezwa na OECD (OECD model treaty) kwani mkataba huu wa kikodi unalinda kampuni kubwa za nje dhidi ya nchi changa kama Tanzania.
(ii) Tanzania ijondoe katika mikataba yote ya kikodi na nchi ambazo ni ‘tax havens’ kama Mauritius, Uingereza (City of London and British overseas territories), Luxembourg, Netherlands n.k.
(iii) Kampuni yoyote ya ndani na nje yenye kampuni dada zilizosajiliwa kwenye ‘tax havens’ zitangaze bayana na kuweka wazi hesabu zao kwa miaka mitano iliyopita kwa ukaguzi wa TRA na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
(iv) Bunge litunge sheria kudhibiti matumizi ya ‘tax havens’ yanayofanywa na kampuni za uwekezaji na haswa kwenye sekta za Mawasiliano, Madini, Mafuta na Gesi na nyinginezo.