Polisi wawili wa Musoma, Mkoa wa Mara na Kibaha, Pwani wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha risasi 3,000 kutoka Musoma kwenda Dar es Salaam.
Wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni aliyekuwa mtunza chumba cha silaha Kikosi cha FFU Musoma na mwenzake mwenye cheo cha Koplo Wilaya ya Kibaha, Pwani. Inadaiwa walikamatwa Juni 2, mwaka huu saa 11:00 alfajiri.
Watuhumiwa wanashikiliwa Kituo cha Polisi Musoma na wamefunguliwa jalada MUS/RB/2465/013 wizi wa risasi 1,056, wanasubiri taratibu zingine za polisi.
Habari zinadai shehena hiyo ilisafirishwa kwa kutumia pikipiki hadi Kituo cha Mabasi, lakini polisi tayari walikuwa wameweka mtego baada ya kupata taarifa kuhusu wizi huo.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo wahusika wa basi na nyumba moja ya kulala wageni iliyopo jirani na stendi, baadhi ya askari waliovaa kiraia walionekana maeneo hayo mapema.
Kwa mujibu wa habari za uhakika kutoka ndani ya polisi, Koplo huyo alikutwa na shehena hiyo karibu na kituo cha mabasi ya Kampuni ya Mohammed Trans, akijiandaa kuelekea Dar es Salaam ambako inasemekana wana wateja wao.
Inadaiwa koplo huyo aliomba ruhusa ya ugonjwa kazini kwake na kuitumia kusafiri hadi Musoma kuchukua mzigo huo, inadaiwa biashara yao hiyo ni ya muda mrefu na wana mtandao na watu wanaojihusisha na uhalifu.
Mtandao huo unadaiwa kuwagusa baadhi ya polisi Mkoa wa Tarime na Rorya, ambao huwauzia watu wanaojihusisha na uhalifu wa kutumia silaha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma alipotafutwa kwa simu zake za mkononi licha ya kuitwa, hazikupokewa.
Hata hivyo, aliomba atumiwe ujumbe, licha ya kupelekewa huo ujumbe, hakujibu ingawa taarifa zinadai ameanza likizo ya kustaafu hivi karibuni.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mara, Jafari Mohammed alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alikanusha kufahamu suala hilo huku akigeuka kuwa mkali kwa mwandishi.
“Hilo mimi silijui, nani kakwambia wewe… askari kukutwa na risasi mfukoni ni jambo la kawaida huenda ni uzembe tunamshughulikia kwa uzembe,” alisema.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment