advert

http://

Saturday, 25 May 2013

Rais Museveni afanya mabadiliko jeshini

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefanya mabadiliko katika makamanda wake wakuu wa jeshi , huku kukiwa na taarifa za kutofautiana kwa majenerali wa jeshi kuhusu ikiwa mwanawe Museveni anaweza kumrithi babake kama rais.
Mkuu wa majeshi, Aronda Nyakairima aliyetajwa katika taarifa iliyofichuliwa kuwa mmoja wa wanaopinga mwanawe Museveni Muhoozi Kainerugaba kumrithi babake, amehamishwa hadi wadhifa wa kiraia kuwa waziri wa mambo ya ndani.
Taarifa za kutofautiana kwa majenerali jeshini ziliibuka mapema mwezi huu wakati magazeti ya Uganda yalipochapisha barua kutoka kwa Generali mkuu David Sejusa Tinyefuza, akidai kuwa Museveni anamtayarisha mwanawe kumrithi atakapoachia ngazi.
Barua hiyo pia inasema kuwa Museveni anapanga kuwaua wale wanaopinga njama yake.
Majenerali kadhaa wakuu walipinga barua ya Tinyefuza wakati kundi la wachache likimuunga mkono.
Mabadiliko katika jeshi yanakuja baada ya magazeti makuu ya upinzani yaliyotoa madai ya mgawanyiko jeshini , yakisalia kufungwa kwa siku ya tano huku polisi wakiendelea kufanya msako katika ofisi zao kuitafuta barua hiyo.
Taarifa ya serikali imesema mabadiliko hayo sio makubwa bali ni madogo katika kuhakikisha serikali inafanya vyema kazi yake.
Hata hivyo msemaji wa jeshi Paddy Ankunda alisema kuwa hayo ni mabadiliko ya kawaida jeshini.
Ankunda alisema kuwa hakuna mgogoro jeshini na kuongeza kuwa Museveni ana haki ya kufanya mabadiliko yoyote kama anavyoridhia.
Mkuu mpya wa majeshi ni Edward Katumba Wamala, ambaye amelimbikiziwa sifa tele kwa kuongoza jeshi la Uganda katika vita dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu (Al Shabaab) nchini Somalia.
Ofisi za magazeti ya Daily Monitor na Red Pepper zilifungwa na kuzuiwa kuchapisha magazeti yoyote na yameendelea kufungwa licha ya agizo la mahakama kutaka polisi kuondoka katika ofisi hizo.Chanzo http://www.bbc.co.uk/swahili/habari

No comments: