advert

http://

Saturday, 29 June 2013

NAIBU MKURUGENZI WA CUF ATEKWA NA WANAUSALAMA HUKO MTWARA


Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge wa Chama Cha Wananchi CUF - Shaweji Mketo ametekwa na wanausalama na wanajeshi waliopiga kambi Mtwara MJINI.

Mketo alienda Mtwara MJINI jana na Leo asubuhi alihudhuria mahakamani ambapo kesi ya Mwenyekiti wa vijana CUF taifa (JUVICUF) Katani Ahmed Katani iliahirishwa.

Baada ya ahirisho hilo, Mketo alikutana na wanachama wa CUF walioko Mtwara MJINI na kufanya nao kikao cha ndani. Katika kikao hicho alielezwa namna wananchi wanavyoteswa kikatili na askari jeshi. Moja ya jambo aliloelezwa ilikuwa ni juu ya mama mmoja aliyebakwa na askari na kisha mamlaka zote zimekataa kumsaidia kuujulisha umma unyama aliofanyiwa.

Mkurugenzi wetu Mketo alipojulishwa jambo hilo aliomba akutane na mama huyo. Baada ya kikao, Mketo na viongozi waandamizi wa wilaya akiwamo mhe. Kulaga ambaye ni katibu wetu wa wilaya walianza safari ya 
kuelekea Msimbati ambako mama huyo amejisitiri baada ya kubakwa na kunyimwa msaada na vyombo vilivyopaswa kumsaidia.

Mketo alifika Msimbati na kukutana na mama huyo na akachukua ushahidi mbalimbali. Wakati wanarudi Mtwara MJINI ndipo walipotekwa na Askari jeshi. Hivi sasa ukipiga simu za Mketo 0782 095 434 na ile ya Kulaga 0789 604968 zote zinapokelewa na askari jeshi na wanajibu kwa matusi ya nguoni na kebehi za Hali ya juu.

Tumefanya juhudi za kuwasiliana na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa polisi na serikali bila mafanikio. Nimempata hewani RPC wa Mtwara ambaye anakiri kuwa hajawashikilia viongozi wetu. Nimemjulisha kama wako mikononi mwa wanajeshi na wanausalama anasema hana mamlaka yoyote juu yao. HII ina maana kuwa mkuu wa Jeshi la polisi wa mkoa Leo hana dhamana ya raia wanaokamatwa na kuteswa katija eneo lake la kazi. Kama Leo Mtwara iko chini ya Jeshi la wananchi na wanatesa watakavyo, Mbona rais hajatangaza Hali ya hatari Mtwara??

Kwa taarifa zenye ushahidi, hadi sasa askari jeshi hao wameshawakamata na kuwapeleka makambini zaidi ya wananchi 100 ambapo wote hao wameteswa kinyama kwa kuvuliwa nguo zote, kumwagiwa maji mwili mzima, kupakwa chumvi mwilini na kuanza kutandikwa viboko vya miti maalum na kisha wakimaliza kuteswa huachiwa na kurudishwa uraiani kuuguza vidonda vinavyotokana na vipigo. Hakuna utawala wa sheria Mtwara, ni ubabe, ukatili na dhuluma. Hakuna mahakama wala JAJI, kila anayedhaniwa kuwa anapaswa kukamatwa lazima atakamatwa na kamwe hapelekwi mahakamani, anateswa kikatili na kuachiwa.

Kwa namna askari waliowashikilia wanavyojibu kikatili, unaweza kupata picha Mketo, Kulaga, dereva Kashinde na yeyote mwingine walivyo chini ya mateso makali ya wanyama hawa.

Tunaposema kuwa nchi hii kuna siku kila mtu atachoka tusilaumiwe. Siku hiyo itakapofika hatutasita kuamuru raia wapambane na askari kila watakapowaona, tutakapofika hapo nchi itabakia vipandevipande. Haiwezekani Leo kusini mwa Tanzania kumegeuka sehemu ya mateso, ukatili na unyama.

Tunaendelea kupambana kwa nguvu kuhakikisha kuwa serikali inawajibika, jeshi linawajibika. Hatutakubali kuona uhuru na utu wa wananchi wa nchi hii unapotezwa kwa faida za watu wachache.

Vyombo vya HABARI hivi sasa haviripoti chochote kuhusu mateso ya wananchi Mtwara. Ripoti za mateso ni Arusha, DSM na Mwanza. Nani atasimamisha ukatili huu wa watu wasio na hatia kama siyo mimi na wewe?

Mawakili wetu pamoja na mimi binafsi tunaelekea Mtwara kesho, lazima haki itendeke na tutaitafuta haki kokote na kwa njia yoyote.

J. Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu,
Chama Cha Wananchi CUF,
Tanzania Bara.
+255717536759.

No comments: