Zaidi ya wanafunzi 300 wa elimu ya juu wa vyuo mbalimbali watakosa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kutokana na kushindwa kujaza fomu za kuomba mikopo katika kipindi kilichowekwa.
Watakaokosa mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo wa 2013/2014 ni kuanzia mwaka wa pili na kuendelea, ambao hawakujaza fomu za kuonyesha taarifa zao mpya kwa bodi. Wanafunzi hao walitakiwa kuwasilisha maombi ya kupewa mikopo kati ya Mei hadi Julai 30, mwaka huu. Mkugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HELSB, Cosmas Mwaisobwa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi kuhusu utendaji wa kazi wa bodi hiyo. Mwaisobwa alisema kwa kuwa wanafunzi hao hawakujaza fomu za kuomba mikopo, mwaka huu hawatapata fursa hiyo na kwamba kwa mujibu wa utaratibu wao, kila mwaka lazima mwanafunzi aombe. Alisema wanafunzi watakaokosa fursa hiyo ya mikopo wameanza masomo yao katika vyuo mbalimbali nchini na kwamba HESLB haijui sababu zilizowafanya wasiombe. Kuhusu ufanisi katika utoaji wa mikopo, Mwaisobwa alisema idadi ya wanafunzi wanaoomba mikopo imeongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/2006 hadi kufikia wanafunzi 97,348 mwaka 2012/2013. Aidha, Mwaisobwa alisema bajeti ya kuwakopesha wanafunzi imeongezeka kutoka Sh. bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi kufikia Sh. bilioni 306 mwaka 20012/2013. Alisema mwaka huu serikali imeitengea bodi hiyo Sh. bilioni 325 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wapya, 31,647 na 62,376 wanaondelea na masomo yao katika vyuo mbalimbali. Wakati wanafunzi hao wakikosa fursa ya mikopo, mapema mwezi huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliitaka bodi hiyo kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi na weledi mkubwa kwa mwaka huu wa masomo ili kuepusha migogoro ya wanafunzi kuhusu mikopo.
CHANZO: NIPASHE
|
MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.
Ametoa kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne, Septemba 24, 2013) mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha.
Mchungaji Mstaafu Mwaisapila maarufu kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa hili.
“Mungu ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.
Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.
Bw. Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.
Aliomba wapatiwe mikopo ya matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa ni jambo linalowezekana kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo ya wilaya (DADPS).
“Andaeni andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea ni jambo linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”
Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.
“Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka kwenu,” alisema.
|
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin tumboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja waliokamatwa kuwa ni Nasri Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa Kigogo Luhanga.
“Kila pipi ina urefu wa sentimita sita...tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu mmoja alifariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga na tukaamua kulifuatilia tukio hilo” alisema.
Alisema makachero walifika eneo la tukio, nyumbani kwa Omari na kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni huku akiwa hana nguo na amefunikwa na shuka.
“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti, alisema marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu Kandunda (43), maarufu kama Mashaka Mabruki” alisema.
Kamishna Kova alisema uchunguzi wa awali, ulionesha kuwa Kandunda alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao wawili.
Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo la madaktari wawili na kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu wa karibu wa marehemu, ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa marehemu, tumboni zilikutwa pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba alikuwa ni mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kabla ya kurudi Tanzania alikuwa akitumikia kifungo nje ya nchi barani Asia” alisema.
Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha marehemu. Alisema wote watakaobainika kuhusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu huyo alikutwa na vielelezo vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola za Marekani 100 na fedha ya Ushelisheli.
Alisema operesheni ya kukamata dawa za kulevya, inaendelea. Aliomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa hizo, kwani zina madhara makubwa kwa wananchi, hasa vijana.
|
No comments:
Post a Comment