advert

http://

Thursday 26 September 2013

AGNESS MASOGANGE AAHIDIWA NDOA MARA ATAKAPOTUA BONGO.



MCHUMBA wa ‘video queen’ maarufu Bongo, Agnes Jerald ‘Masogange ‘, Evance Komu amefungua kinywa chake na kusema; siku mchumba wake huyo atakapotia miguu nchini, wanafunga ndoa.

Masogange kwa sasa yupo nchini Afrika Kusini alikokuwa akikabiliwa na kesi ya madawa ya kulevya ambapo alifanikiwa kuwa huru baada ya kulipia faini ya randi 30,000 (shilingi 4,800,000) aliyoamriwa na Mahakama ya Kempton.


Akizungumza hivi karibuni mara baada ya Masogange kuachiwa, Evance alisema anamshukuru Mungu kwa kesi hiyo kumalizika na kinachofuata kwenye uchumba wao ni ndoa tu.


Evance aliweka bayana kuwa kinachomsukuma afanye uamuzi huo kwa sasa ni kutokana na jinsi alivyoguswa na changamoto kubwa alizopitia mchumba wake hivyo ameona kuna kila sababu ya kumuoa kabisa ili apate faraja ya milele.


“Mchumba wangu amepitia majaribu ya kutosha na mimi sioni muda wa kupoteza tena, akitua tu Bongo kinachofuata ni ndoa nina imani itakuwa ndiyo jambo kubwa la kumfariji na kumpa upendo wa hali ya juu,” alisema Evance pasipo kutaja siku ambayo mchumba wake atarejea.


Katika kesi hiyo iliyokuwa ikimkabili Masogange, alishikiliwa na mwenzake Melisa Edward ambaye naye aliachiwa huru kwa kukosekana na hatia.



Klabu moja ya Qatar inataka kumsajili Mrisho Ngassa kwa mkataba wa miaka miwili.

Mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Yanga wanaweza kumkosa mshambuliaji wao mahiri Mrisho Ngassa baada ya klabu moja ya Qatar kuonyesha nia ya kumsajili huku mchezaji huyo akikiri kwamba  dau walilomuahidi linamshawishi.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi ilizipata jana zilisema kuwa, tayari Ngassa amekwishafanya mazungumzo na klabu hiyo ambayo ipo tayari kuilipa Simba SC milioni 45 anazodaiwa na kuifidia Yanga kwa kumuuza mchezaji huyo.
Taarifa hizo zimesema kuwa klabu hiyo inataka kumtumia Ngassa baada ya usajili wa dirisha dogo.Ngassa alithibitisha hilo huku akikataa kutaja jina la timu hiyo kwa sababu za kisheria za usajili wa wachezaji na kuogopa adhabu ya Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa).
Mchezaji huyo alikiri kuwa timu hiyo ipo tayari kumpa mkataba wa miaka miwili na kuzilipa Simba SC na timu yake ya sasa, Yanga.
Alisema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuona suala lake la kuitumikia Yanga katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara linashika sura mpya kutokana na mvutano wa malipo.
Alifafanua kuwa klabu hiyo imemuahidi donge nono na kuamua kufuta msimamo wake wa zamani wa kutaka kucheza soka hapa nchini kutokana na maslahi anayopata.
“Maslahi yao mazuri na mazingira waliyoniahidi kimkataba, nimevutiwa nao kutokana na ukweli kuwa suala langu la kuichezea Yanga limekumbwa na vipingamizi vingi,” alisema Ngassa.
Alisema kuwa baadhi ya wadau wa Yanga na marafiki zake wana nia njema ya kutaka kumlipia fedha anazodaiwa na Simba, lakini uongozi wa Yanga bado haujatoa jibu la sakata hilo.
“Nimemaliza kifungo cha mechi sita, sasa suala lililobaki ni malipo, viongozi hawajatoa jibu mpaka sasa, ” alisema Ngassa.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga alikiri kuwa bado hawajailipa Simba fedha wanazomdai Ngassa kutokana na majadiliano waliyokuwa nayo.
Sanga alisema kuwa wana uhakika kuwa Ngassa ambaye anafanya mazoezi ya nguvu na Yanga, atacheza Jumamosi dhidi ya timu ngumu ya Ruvu Shooting.
Source:Mwananchi.

Anaitwa SaRaha na huu hapa Chini ni wimbo wake
 unaitwa Mbele Kiza.Kaimba Vizuri kuliko hata wasanii wa Kibongo.Isikilize na kuidownload.

MSHAMBULIAJI Mrisho Ngassa wa Yanga, ameuambia uongozi wake yupo tayari ulilipe Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kitita cha Sh milioni 45 kutoka kwenye mshahara wake.

Ngassa amekubali kitita hicho cha fedha kitolewe kwa kuwa ana hamu ya kuanza kuitumikia Yanga baada ya kumaliza adhabu ya kutocheza mechi sita aliyopewa na TFF.

Imeelezwa Ngassa yupo tayari kukatwa katika mshahara wake na kuna taarifa katika Sh milioni 2 kila mwezi, atakatwa Sh 500,000.


Mshambuliaji huyo alisimamishwa mechi sita pamoja na kutakiwa kurudisha Sh milioni 30 alizolipwa na Simba pamoja na faini ya Sh milioni 15. TFF ilishikilia msimamo wake kwamba Ngassa hatacheza hadi atakapolipa fedha hizo za Simba.


Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Ngassa amekubali kuhusiana na hilo na alifikia makubaliano hayo na mwenyekiti, Yusuf Manji walipofanya kikao walipokutana jijini Mbeya, hivi karibuni.


Alipoulizwa kuhusiana na hilo jana, Ngassa alisema:  “Sawa, adhabu yangu ya kutocheza mechi sita za mashindano imemalizika, lakini siwezi kuongelea lolote, mimi ni mchezaji tu, kazi yangu ni ndani ya uwanja, hayo mengine ya kiutawala ni vyema yakatolewa ufafanuzi na viongozi,” alisema Ngassa.


Championi Jumatano lilimtafuta Manji ambaye alikiri kuzungumza na Ngassa kuhusiana na masuala kadhaa ya klabu yao likiwemo hilo.
“Mimi ni mwenyekiti, hakuna ubaya kuzungumza na Ngassa. 

Tunazungumza kwa ajili ya klabu yetu, hivyo msubiri akicheza mtamuona,” alisema Manji.

Taarifa nyingine zilieleza kuwa, Yanga ilikuwa tayari kupeleka fedha hizo leo, lakini ilitaka TFF wakate Sh milioni 45 katika Sh milioni 70 inazowadai na walikuwa katika mazungumzo katika hilo.
Kwa upande mwingine, Kocha Mkuu, Ernie Brandts, alisisitiza kwamba ana kila sababu ya kumpanga Ngassa kama atakuwa amerejea katika kikosi watakapoivaa Ruvu Shooting Jumamosi.
“Tuko naye kikosini kila siku, tunafanya naye mazoezi na tunashirikiana. Kama amerejea na yuko katika afya nzuri, nitampanga maana ninamhitaji,” alisema Brandts.
Wakati hilo la Ngassa linamalizika, taarifa nyingine za uhakika zimeeleza Manji alitarajia kukutana na kikosi kizima cha Yanga, jana usiku.
Mwenyekiti huyo alipanga kukutana na wachezaji na benchi la ufundi katika hoteli ya Serena jijini Dar ili kula chakula cha usiku na baadaye kujadili masuala kadhaa kikiwemo kipigo cha Azam FC na nini cha kufanya baada ya hapo ili kusonga mbele na ikiwezekana kutetea
-GPL

INGAWA duka la Westgate liko karibu dakika 15 tu kutoka nyumbani kwangu, nilikuwa nikienda kule kwa nadra kununua vitu. Mara kwa mara huwa kuna watu wengi katika duka hili katika siku za mwisho mwa wiki na hivyo niliona kama karaha. Jumamosi ilikuwa maalumu kwa sababu nilitaka kutumia muda wangu na mkwe yangu, Amina (si jina halisi) na baadhi ya marafiki zetu ambao watoto wao walikuwa wakishiriki katika shindano la upishi.


Tulikuwa juu ya ghorofa la mwisho saa 5.00 asubuhi. Shindano la upishi lilikuwa likiendelea. 

Baada ya muda, Amina aliamua kuelekea chini kwa ajili ya kununua vitafunwa. Sikuwa na njaa sana hivyo niliamua kubaki hapo hapo. Nilitaka kuangalia watoto wakipika.

Karibu saa saba na robo, Amina alikuwa hajarejea nilipokuwa, lakini sikuwa na hofu na nilibakia hapo hadi niliposikia sauti ya milio ya bunduki.

Nilishikwa na kihoro na kumpigia simu mwanangu. Ni ofisa usalama na nilidhani pengine angeweza kusaidia.

“Kuna milio ya risasi hapa. Naweza kusikia milio ya risasi. Tafadhari fanya unaloweza,” nilimwambia.

Niliongea naye kwa muda mfupi kwa simu kwa sababu nilitaka kuzungumza na mkwe wangu. Katika simu aliniambia kuwa alikuwa amejificha katika benki iliyo kwenye kituo hicho cha biashara. Alisisitiza kwamba yu salama na alitaka niwe mwangalifu.

Mazungumzo yetu yalihitimishwa ghafla nilipoona watu wawili wakija juu. Walikuwa na bunduki na haikunichukua muda nikaona mabomu ya kutupwa kwa mkono yakining’inia katika mikanda yao.

Nyuso zao hazikufichwa na tuliziona wazi kana kwamba walikuwa hawajali iwapo tungeweza kuwatambua baadaye. Mara moja nilianza kuwa na wasiwasi huenda nisitoke hai.

Katika kitambo hicho, hofu yangu ilikuwa kubwa. Magaidi walipoanza kurusha risasi na magurunedi holela, umati ukaangua kilio kwa kihoro. 

Watu walianza kukimbia kwa mshtuko huku mwelekeo wao ukiwa haueleweki. Nami nilikimbilia katika hema lililokuwa likitumika kama jiko la watoto na kujificha humo.

Awali nilidhani walikuwa wakifyatua risasi kwa bahati mbaya. Hata hivyo, punde nikaona kwamba wale watu waliokuwa wakikimbia huko na huko wakipiga kelele ni wale waliokuwa wamepigwa risasi. Huku kukiwa na makelele, niliwasikia magaidi wakiwaita Waislamu:

“Kama ninyi ni Waislamu, mnaweza kunyanyuka na kuondoka,” walisema.

Lakini haikuwa rahisi kama ilivyodhaniwa. Waislamu walitakiwa kuthibitisha imani yao. Walitakiwa kutaja jambo fulani kutoka aya za Korani kabla ya kuachiwa. Na hata baada ya hapo bado unaweza kupoteza maisha yako. Mwanamke mmoja ambaye alisema alikuwa Muislamu lakini hakuonekana kuwa Muislamu alipigwa risasi na kufa.

Sina uhakika kwa nini sikutumia dini yangu ili kujiokoa mapema. Pengine ilitokana na hofu. Pengine ilitokana na hali ya ukaidi.

Nikiwa nimejificha nyuma ya maboksi na meza katika hema, watu nisiowajua wakawa wa karibu nami kuliko marafiki. Magaidi lazima walijua tulipo; kulikuwa na maeneo mengi ambayo tungeweza kuyatumia kujificha.

Hata hivyo, tulitulizana wenyewe kwa wenyewe huku tukiwataka watoto wanyamaze kwa sababu sauti zingeweza kutufichua pale tulipo. 

Lakini pamoja na juhudi zetu zote za kuwatuliza wanyamaze, bado baadhi ya watoto hawa hasa wale wadogo walilia.

Tuliomba. Tuliwasilisha maombi yetu kimyakimya kwa Muumba wetu, pengine tukiona hiyo ni siku yetu ya mwisho kuwa hapa duniani.

Tulikuwa tumejificha kwa dakika 20 wakati nilipomsikia mmoja wa magaidi akipokea simu kupitia simu yake ya mkononi. Hakuzungumza kwa sauti kubwa, lakini ilikuwa sauti tulivu ya Kiswahili iliyosikika vema masikioni.

Maneno halisi ilikuwa vigumu kuyakumbuka. Lakini alisema kuwa ameua watu wengi na wengine zaidi walijeruhiwa.

Dakika chache baadaye baada ya kupokea simu, magaidi walirusha risasi ovyo juu ya paa na kuondoka. Nikadhani kwamba milio hiyo ya mwisho ililenga kutuogopesha na kutuonya tusijaribu kuondoka mahali tulipo.

Tuliokolewa muda mfupi baadaye na wakati nikitembea kutoka katia jengo hilo tuliona miili ikiwa imezagaa sakafuni, nilijisikia nisiye na msaada kwamba sikuweza kufanya lolote kuzuia hali hii. 

Nilikuwa huru lakini mkwe wangu alikuwa bado amenasa katika jengo. Nilipompigia simu alinihakikishia kuwa yu salama tena kwa sauti tulivu. Alinitaka nisiwe na wasiwasi, ombi ambalo halikuwezekana kwangu.

Amina aliokolewa saa 12 jioni. Saa kadhaa nikiwa nyumbani kwa mwanangu na kwa rafiki yangu kusubiri neno la matumaini kutoka kwake ilikuwa tete hakika.

Nilifarijika sana wakati alipompigia simu mwanangu akimtaka aende kumchukua kutoka Visa Oshwal.

Saa zaidi ya 24 baada ya ile iliyokuwa siku njema nikiwa na mkwe wangu iligeuka kuwa jinamizi, na bado ninatetemeka nikiikumbuka. Hata hivyo, nina furaha kuwa hai na ninashukuru Amina na mimi tulitoka Westgate bila majeraha.

*Hii ni simulizi ya mmoja wa watu waliookoka katika tukio la ugaidi la Westgate

MAMA wa aliyekuwa msanii maarufu Bongo, marehemu Hussein Mkiety ‘Sharo Millionea’, Zainab Mkiety amemkataa mtoto ambaye alipelekewa Tanga na mama yake anayetokea Geita akidai ni damu ya Sharo.


Mtu wa karibu na familia hiyo amesema kuwa baada ya msiba kupoa, mama wa mtoto huyo alifunga virago na mwanaye kwa ajili ya kwenda kutembelea kaburi la Sharo na kwenda kujitambulisha kwa bibi wa mtoto.


Chanzo hicho kilieleza kuwa mama mtoto huyo alipofika Muheza jijini Tanga, alipokelewa na watu wa bodaboda ambao walimsindikiza hadi nyumbani kwa mama Sharo.


“Alipofika alipokelewa lakini cha kushangaza mama Sharo alimkataa na kusema marehemu hakuwa na mtoto kwa sababu hakuwahi kumwambia,” alisema sosi huyo.

Ili kupata ukweli wa habari hiyo, paparazi wetu aliwasiliana na mama Sharo kwa simu ambapo alikuwa na haya ya kusema:


“Ni kweli alikuja mwanamke akiwa amebeba mtoto ambaye alijitambulisha kwangu kuwa ametokea Geita.


“Alisema mtoto aliyekuwa amembeba ni wa Sharo lakini nilikataa nikamwambia kuwa mwanangu hakuwahi kuniambia kuwa ana mtoto na nilipowauliza marafiki zake walisema hawana taarifa hizo.


Nisingeweza kumpokea kwa sababu alishajitokeza mwingine na kudai kuwa ana mimba ya mwanangu, baada ya kumkataa mwanamke huyo aliondoka na mpaka leo sina mawasiliano naye.”


Sharo alifariki dunia kwa ajali ya gari Novemba 26, mwaka jana katika Kijiji cha Maguzoni-Songa, Wilaya ya Muheza jijini Tanga.

GPL

WANAFUNZI 300 ELIMU YA JUU KUKOSA MIKOPO.


Zaidi ya wanafunzi 300 wa elimu ya juu wa vyuo mbalimbali watakosa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kutokana na kushindwa kujaza fomu za kuomba mikopo katika kipindi kilichowekwa. 

Watakaokosa mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo wa 2013/2014 ni kuanzia mwaka wa pili na kuendelea, ambao hawakujaza fomu za kuonyesha taarifa zao mpya kwa bodi. 
Wanafunzi hao walitakiwa kuwasilisha maombi ya kupewa mikopo kati ya Mei hadi Julai 30, mwaka huu.
Mkugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HELSB, Cosmas Mwaisobwa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi kuhusu utendaji wa kazi wa bodi hiyo. 
Mwaisobwa alisema kwa kuwa wanafunzi hao hawakujaza fomu za kuomba mikopo, mwaka huu hawatapata fursa hiyo na kwamba kwa mujibu wa utaratibu wao, kila mwaka lazima mwanafunzi aombe. 
Alisema wanafunzi watakaokosa fursa hiyo ya mikopo wameanza masomo yao katika vyuo mbalimbali nchini na kwamba  HESLB haijui sababu zilizowafanya wasiombe. 
Kuhusu ufanisi katika utoaji wa mikopo, Mwaisobwa alisema idadi ya wanafunzi wanaoomba mikopo imeongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/2006 hadi kufikia wanafunzi 97,348 mwaka 2012/2013. 
Aidha, Mwaisobwa alisema bajeti ya kuwakopesha wanafunzi imeongezeka kutoka Sh. bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi kufikia Sh. bilioni 306 mwaka 20012/2013. 
Alisema mwaka huu serikali imeitengea bodi hiyo Sh. bilioni 325 kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wapya, 31,647 na 62,376 wanaondelea na masomo yao katika vyuo mbalimbali. 
Wakati wanafunzi hao wakikosa fursa ya mikopo, mapema mwezi huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliitaka bodi hiyo kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi na weledi mkubwa kwa mwaka huu wa masomo ili kuepusha migogoro ya wanafunzi kuhusu mikopo.


CHANZO: NIPASHE

MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.


Ametoa kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne, Septemba 24, 2013) mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha.

Mchungaji Mstaafu Mwaisapila maarufu kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa hili.

“Mungu ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.

Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.

Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.

Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.

Bw. Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.

Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.

Aliomba wapatiwe mikopo ya matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa ni jambo linalowezekana kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo ya wilaya (DADPS).

“Andaeni andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea ni jambo linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”

Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.

“Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka kwenu,” alisema.

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin tumboni.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja waliokamatwa kuwa ni Nasri Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa Kigogo Luhanga.

“Kila pipi ina urefu wa sentimita sita...tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu mmoja alifariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga na tukaamua kulifuatilia tukio hilo” alisema.

Alisema makachero walifika eneo la tukio, nyumbani kwa Omari na kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni huku akiwa hana nguo na amefunikwa na shuka.

“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti, alisema marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu Kandunda (43), maarufu kama Mashaka Mabruki” alisema.

Kamishna Kova alisema uchunguzi wa awali, ulionesha kuwa Kandunda alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao wawili.

Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo la madaktari wawili na kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu wa karibu wa marehemu, ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa marehemu, tumboni zilikutwa pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya mamilioni ya fedha.

“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba alikuwa ni mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kabla ya kurudi Tanzania alikuwa akitumikia kifungo nje ya nchi barani Asia” alisema.

Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha marehemu. Alisema wote watakaobainika kuhusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu huyo alikutwa na vielelezo vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola za Marekani 100 na fedha ya Ushelisheli.

Alisema operesheni ya kukamata dawa za kulevya, inaendelea. Aliomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa hizo, kwani zina madhara makubwa kwa wananchi, hasa vijana.